ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, December 2, 2025

DC KIBAHA AKABIDHI GARI LITAKALOTUMIKA KUBORESHA HUDUMA KATIKA DIVISHENI YA ARDHI

 

NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon,(Hapo Juu Pichani Kushoto) amekabidhi rasmi gari jipya kwa Divisheni ya Ardhi na Mipango Miji, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi katika utatuzi wa changamoto za ardhi.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mhe. Simon alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka kipaumbele katika utatuzi wa migogoro ya ardhi na upatikanaji wa maeneo ya viwanda na uwekezaji.

“Hili gari limeletwa ili muweze kuwafikia wananchi kwa haraka na kuhakikisha changamoto za ardhi zinatatuliwa kwa wakati. Nawaomba mlitunze na mlitumie kwa kazi iliyokusudiwa,” alisema Mhe. Simon, huku akimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa kutekeleza maagizo kwa ufanisi.

Awali, akiwasilisha taarifa fupi, Dkt. Shemwelekwa alibainisha kuwa gari hilo linathamani ya shilingi milioni 170, na litakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza kasi ya utoaji huduma bora hususan katika Divisheni ya Ardhi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Ardhi, Denis Kahumba, amesema changamoto ya usafiri ambayo ilikua ikikwamisha utendaji sasa imepatiwa ufumbuzi.

“Ahadi yangu ni kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tunashukuru kwa vitendea kazi na mazingira mazuri ya kazi ambayo yameongeza morali kwa watumishi,” alisema Kahumba.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Rugambwa Banyikila, ametoa pongezi kwa uongozi wa Manispaa ya Kibaha kwa kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili ofisi ya ardhi na kuwataka watumishi kuongeza bidii na uwajibikaji.

Makabidhiano haya yanatarajiwa kuongeza kasi ya usimamizi wa ardhi, kutatua migogoro, na kuimarisha huduma kwa wananchi wa Kibaha, huku yakiendana na dira ya Serikali ya kujenga mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo.

DR. NICAS KUNOGILE AKWEA PIPA NAFASI YA UMEYA HALMASHAURI MANISPAA YA KIBAHA

 


Na Victor Masangu,Kibaha 


Diwani mteule wa Kata ya Tumbi  Dkt. Nicas Mawazo amechaguliwa kuwa Meya mteule wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha baada ya kupata kura 15 kati ya kura halali zipatazo  19 ambazo zimepigwa na madiwani  wateule wa chama cha mapinduzi (CCM)  huku Aziza Mruma akichaguliwa kuwa katika nafasi ya Naibu meya kwa kupata kura 10 .

  Akitangaza matokeo hayo ya uchaguzi wa ndani wa chama Katibu wa Chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Issack Mawazo amebainisha kwamba zoezi zima uchaguzi huo umemalizika  salama na kwamba viongozi  hao wateule wanatarajiwa kuapisha Disemba 4 mwaka huu  

Katibu huyo amefafanua kuwa zoezi hilo la uchaguzi limekwenda vizuri na kwamba  wagombea wote wameridhishwa na matokeo hayo na kuwahimiza viongozi hao kuvunja makundi na badala yake wawatumikie wananchi.


Kwa upande wake Meya mteule kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM ) Dr,Nicas Mawazo  amesema kwamba uchaguzi huo umeendeshwa kwa haki na uhuru na kwamba matarajio yake makubwa ni kushirikiana na madiwani wenzake katika kuwaletea chachu ya maendeleo ikiwa pamoja na kuwapambania wananchi walio wanyonge.

 Naye Naibu Meya mteule  waa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma amesema kuwa lengo lake kubwa ni kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Viongozi hao waliochaguliwa katika nafasi za Meya na Naibu Meya   Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wanatarajiwa kuapishwa rasmi  Disemba 4 mwaka huu.

Monday, December 1, 2025

NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI ATOA MAAGIZO KWA WAKURUGENZI JUU YA KAMPENI YA KUWAPELEKA WATOTO SHULE

MWANDISHI:- VICTOR MASANGU, PWANI MTANGAZAJI:- ALBERT G.SENGO Naibu waziri Ofisi ya Waziri mkuu Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Reuben Kwagilwa anayeshugulikia masuala ya elimu amewaagiza wakurugenzi wote nchi nzima kufanya kampeni kwa ajili ya kuwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka na kuwaandikisha watoto wao shule za awali na msingi pindi ifikapo Januari mwaka 2026, Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo ameweza kugagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambayo imejengwa katika eneo la Disunyara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kumwagiza mkandarasi kumaliza mradi huo kwa muda uliopangwa.

Sunday, November 30, 2025

STANBIC BANK MWANZA YAFANYA KWELI SEKTA YA AFYA MWANZA

 NA. ALBERT G.SENGO/MWANZA

Benki ya Stanbic imeonesha tena dhamira yake ya kusaidia jamii kwa vitendo, baada ya kukabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 19 kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza. Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na vitanda vya wagonjwa, mashuka na viti mwendo, vitapelekwa katika Hospitali za Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, ili kusaidia katika utoaji wa huduma bora za afya. Kutoka kwa mwanahabari wetu Albert G. Sengo., anashuka na taarifa kamili

Wednesday, November 26, 2025

DKT. MWIGULU AWAONYA WAVUNJIFU WA SHERIA

 WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani vitekeleze sheria hizo bila upendeleo kwani tabia ya kuogopana na kuoneana aibu imechangia baadhi ya watu kukwepa wajibu wakati wengine wakibebeshwa mzigo wa sheria.


“Yeyote atakayevunja sheria akamatwe na hatua zichukuliwe kwa usawa. Huyu mmoja anavunja sheria anakamatwa, analipa. Huyu mwingine anavunja mbele yake anaachwa. Kama una haraka, toka mapema zaidi si kufidia kwa kuvunja sheria.”

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Novemba 26, 2025) wakati akifungua Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa haitakuwa uungwana kuona baadhi ya watu wakilipa adhabu papo hapo wanapokosea ilhali wengine wakiachwa kupita bila kuchukuliwa hatua.

Amewaonya baadhi ya viongozi na madereva wa Serikali ambao wanaelewa sheria vizuri lakini bado wanazikiuka kwa makusudi. “Ni muhimu kuwasaidia watumiaji wa vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji ambao kwa sehemu kubwa wanaweza kuwa hawazielewi sheria kikamilifu, badala ya kuwaadhibu kwa upendeleo.”

Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kuwapa Watanzania wote heshima na kuhakikisha sheria zilizowekwa zinatekelezwa kwa maslahi ya wote na kuongeza kuwa endapo zipo sheria ngumu kutekelezeka, basi zibadilishwe ili kila Mtanzania anufaike.


Ameviagiza vyombo vya usimamizi wa sheria vihakikishe kuwa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri wanazingatia usimamizi wa sheria na kuchukua hatua kwa yoyote anayevunja sheria akamatwe na kuchukuliwa hatua bila kuonewa aibu.

“Inaudhi mtu amebeba mgonjwa anafuata sheria, halafu mwingine anapita tu anavunja sheria, hapati adhabu. Mlalahoi akivunja sheria anapata adhabu, tunawapa kazi watekeleza sheria kuwaomba radhi watu waliovunja sheria. Naelekeza kila mtu afuate sheria, uwe wa serikalini ama uwe binafsi, tumeweka sheria, zifuatwe kama zilivyo.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema sekta ya uchukuzi ni mojawapo ya sekta wezeshi za uchumi duniani kota na kwamba watu wanahitaji njia za uchukuzi ili kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wa usafirishaji nchini ili kuhakikisha masuala ya nishati safi yanapewa kipaumbele. Akitoa mfano, Waziri Mbarawa alisema: “Uendeshaji wa reli ya kisasa (SGR) unatumia nishati ya umeme, mabasi ya mwendokasi njia ya Mbagala yanatumia gesi asili na baadhi ya taxi na bajaji zinatumia gesi asili.”

Tuesday, November 25, 2025

WATAALAM WA KIMATAIFA WATOA MWELEKEO MPYA WA UCHUMI KATIKA KONGAMANO LA TIA MWANZA


TIA Yasistiza Utafiti na Ubunifu Katika Kuchochea Uchumi – Kongamano la Kimataifa la 4 la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi Lafana Mwanza

Mwanza, 25 Novemba 2025 – Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) leo imeongoza Kongamano la 4 la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi, lililofanyika katika Ukumbi wa Nyerere, Gold Crest Hotel jijini Mwanza, likiwa na ujumbe mahsusi unaoangazia nafasi ya ubunifu, uvumbuzi na biashara katika kuchochea uchumi endelevu.


Akizungumza kumwakilisha mgeni Rasmi, Benjamin Magai ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali , amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, kama njia ya kutoa suluhisho la changamoto za kijamii na kiuchumi. Akibainisha kuwa utafiti ndio injini ya maendeleo, hasa katika maeneo kama ubunifu, teknolojia, tathmini, miundombinu na mikakati ya maendeleo yenye tija.


Dira ya Maendeleo ya 2050 Yawekwa 

Dhima: Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu

Kongamano la mwaka huu limebeba kaulimbiu “Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu.” Kaulimbiu hiyo imegawanywa katika mada 11, huku machapisho 41 ya tafiti yakitarajiwa kuwasilishwa.

Prof. Pallangyo alisema kuwa kabla ya mawasilisho ya tafiti, kutakuwa na watoa mada wakuu 8 (Keynote Speakers) kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambao ni wabobezi katika nyanja zao. Miongoni mwao ni:

Watoa Mada Wakuu ni kama ifuatavyo:-

Ephias Ruhode (Uingereza) – Amefafanua namna mkakati wa biashara unavyopaswa kuongoza kabla ya teknolojia, hasa katika zama za Akili Bandia (AI) kupitia mada “In the Age of AI, Business Strategy Comes Before Technology.”
Gaoua Abdelouahab (Algeria) – Ameeleza namna mabadiliko ya kidigitali na ujasiriamali yanavyoweza kuwa injini ya mapinduzi ya kiuchumi, akichambua “The Algerian Experience.”
Prof. Oksana Kiseleva (Urusi) – Amesisitiza umuhimu wa Ecosystem za Ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi duniani.
Dkt. Collin Kamalizeni (Afrika Kusini) – Amejadili nafasi ya uongozi shirikishi katika kuponya majeraha ya uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mada “Reimagining Inclusive Leadership as a Catalyst for Economic Recovery in Sub-Saharan Africa.”

Prof. Tandy Lwoga (Tanzania)
– Amezindua mjadala juu ya jinsi ubunifu unavyoungana na ujasiriamali katika muktadha wa mifumo ya kidijitali kupitia mada “Innovation Meets Entrepreneurship: Rethinking Digital Collection Development for the Future-Ready User.” 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Pallangyo,  amekumbusha kuwa TIA ni mojawapo ya taasisi kongwe na muhimu nchini katika kutoa elimu ya uhasibu, ugavi na fani nyingine za biashara. Ikiwa na kampasi 8 nchini na zaidi ya wanafunzi 32,000, na taasisi hiyo imeendelea kuimarisha mfumo wa mafunzo unaozingatia umahiri (Competence Based Training – CBET), sambamba na kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.

Akimkaribisha Profesa Goodluck Urassa kutoa salamu za Bodi, viongozi wote wametia mkazo umuhimu wa TIA kuendelea kuwa kichocheo cha sera na maarifa kwa taifa.

Baada ya mawasilisho ya tafiti, TIA imetangaza kuwa itachapisha kitabu maalum kitakachokusanya mapendekezo ya watafiti juu ya namna bora ya kutatua changamoto katika sekta za biashara na uchumi. Kitabu hicho kitasambazwa kwa wadau muhimu, ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama mchango wa TIA katika kusaidia sera na maamuzi ya maendeleo.


Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza utalii, washiriki wa kongamano wamepangiwa kutembelea vivutio vya Jiji la Mwanza. Hii ni sehemu ya mkakati wa kutumia kongamano kama nyenzo ya kuhamasisha utalii wa ndani.






Monday, November 24, 2025

UBUNIFU WA KIPEKEE KISIWA CHA SAANANE WAIBUKA A TUZO

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msadizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, akipokea Tuzo ya Ubunifu wa Mazao ya Utalii, jijini Dar es Salaam.

Ubunifu wake wa kipekee umevuka mipaka ya kawaida na sasa umetambuliwa kitaifa!

 
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza, Dkt. Tutindaga George, ametwaa Tuzo Maalum ya Ubunifu wa Mazao ya Utalii kama sehemu ya Top 100 Executives List Awards 2025.

Katika hafla ya heshima iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2025, Dkt. Tutindaga alitangazwa rasmi kuwa  
"Chief Innovation / Head of Product Design and Innovation of the Year."

Mazao ya Utalii Yaliyompa Tuzo
Kupitia kazi yake katika Hifadhi ya Saanane, Dkt. Tutindaga amebuni na kuboresha bidhaa kadhaa za kipekee za utalii, zikiwemo:  
• Boat Safari katika Ziwa Victoria
• Rock Hiking
• Maeneo ya mapumziko ya kisasa (picnic sites) 
• Michezo ya majini
• Kutazama machweo ya jua
• Uboreshaji wa malazi ya kitalii
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, akionesha Tuzo yake ya Ubunifu wa Mazao ya Utalii.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Tutindaga aliwashukuru wote waliomuunga mkono na kutoa mwito kwa Watanzania kutembelea vivutio vyetu vya asili:

“Nashukuru sana kupata nafasi hii. Kama Mhifadhi, naendelea kuwakaribisha kutembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.”

 Aliongeza kwa kumshukuru Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Kuji, kwa kuendeleza mazingira wezeshi kwa wanawake katika uongozi na ubunifu:

“Tuzo hii si yangu peke yangu, ni heshima kwa TANAPA nzima, ushahidi kuwa ubunifu unazaa matokeo.”

Hifadhi zetu ni hazina ya Taifa
Kila unapozitembelea, unachangia uhifadhi, uchumi na maendeleo ya jamii.  

 


SIMBA SC YACHAPWA 1-0 NA PETRO DE LUANDA LIGI YA MABINGWA DAR

 

TIMU ya Simba SC imeanza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa bao 1-0 na Petro de Luanda ya Angola katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D jioni ya Jumapili ya tarehe 23 Nov 2025 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.


Bao pekee lililoizamisha Simba SC limefungwa na kiungo Mreno, Bernardo Oliveira Dias dakika ya 78 alipofumua shuti la umbali wa Nita 20 ambalo lilimbabatiza beki raia wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck na kubadili njia likimpoteza mwelekeo kipa namba moja Tanzania, Yakoub Suleiman Ali.


Mechi nyingine ya Kundi D jana Espérance ililazimishwa sare ya bila mabao na Stade Malien ya Mali Uwanja wa Hammadi Agrebi, Tunisde Jijini Tunis nchini Tunisia.


Mechi zijazo Simba SC itasafiri kuwafuata Stade Malien Novemba 29 Uwanja wa Machi 26 Jijini Bamako nchini Mali, wakati Petro de Luanda wanarejea nyumbani kuwakaribisha Espérance de Tunis November 29. Uwanja wa Novemba 11 Jijini Luanda.

MUDATHIR APANDA JUKWAANI KUMFUATA RAIS ENG. HERSI BAADA YA GOLI LA DUBE

 

 
WENYEJI, Yanga SC wameanza vyema hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco jioni ya Jumamosi ya Tarehe 22 Novemba 2025 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. 

Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee katika mchezo huo wa kwanza wa Kund B, mshambuliaji wa Kimataifa wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube dakika ya 58 akimalizia pasi ndefu ya kiungo mzawa, Mudathir Yahya Abbas.

Hii inakuwa mara ya kwanza kihistoria Yanga kushinda mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1998.

Saturday, November 22, 2025

CLEMENCE MWANDAMBO ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limethibitisha kumkamata mwalimu wa shule ya awali ya Saint Clemence, baada ya madai ya kusambaza maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi kupitia mitandao ya kijamii. 

Taarifa hiyo imetolewa rasmi na Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, ikisema kuwa tukio hilo limefanyika tarehe 21 Novemba 2025 katika eneo la Uzunquni “A”, jijini Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtuhumiwa alikamatwa majira ya saa 5:20 asubuhi, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa polisi kwamba alikuwa ametumia kurasa zake za “Facebook” na “Instagram” kuchapisha taarifa zilizodaiwa kuhamasisha taharuki na kuweza kusababisha uvunjifu wa amani. Polisi wamesema mara baada ya kupokea taarifa hizo, waliendesha uchunguzi wa haraka ambao ulipelekea hatua ya kumkamata kwa ajili ya kuendelea na mahojiano.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mitandao ya kijamii imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha kusambaa kwa taarifa mbalimbali, hivyo wananchi wanatakiwa kutumia majukwaa hayo kwa uangalifu na kufuata sheria za nchi. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, hatua kali zitachukuliwa kwa watu wote watakaobainika kutumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu, kuhatarisha usalama wa raia au kusambaza taarifa zisizokuwa sahihi zinazoweza kuathiri ustawi wa jamii.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika. 

Hata hivyo, polisi wamesisitiza kuwa hatua hii haikusudiwi kuzuia uhuru wa raia kujieleza, bali inalenga kuhakikisha uhuru huo unatumika kwa kufuata misingi ya sheria na kuheshimu haki za watu wengine.

Aidha, Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kutoa ushirikiano pindi wanapobaini matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ikiwemo uchochezi, uongo, matusi, au taarifa zinazoweza kuleta mgawanyiko katika jamii. 

Lengo lao ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu, huku maendeleo ya teknolojia yakitumika kwa manufaa.

Kukamatwa kwa mwalimu huyo kumeibua mijadala mitandaoni, baadhi ya wananchi wakisema kuwa vyombo vya habari na mamlaka zinapaswa kufafanua zaidi kuhusu ni aina gani ya maneno yanaweza kufasiriwa kama uchochezi ili kuepusha mkanganyiko. 

Wengine wamepongeza hatua za polisi wakisema zinasaidia kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo yameongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesisitiza kuwa litatoa taarifa zaidi endapo kutakuwa na maendeleo mengine kuhusu kesi hiyo, huku likiwataka wanachama wa mitandao ya kijamii kuzingatia maadili na sheria wakati wa kuchapisha au kushiriki taarifa mtandaoni.

HAKIMU AKATAA KUTUPA JELA MWANAFUNZI ALIYEFIKISHWA KORTINI KWA KUIBA POMBE.


 
Mahakama ya Thika imevuta hisia za umma baada ya Hakimu Mkuu Stella Atambo kukataa kumhukumu kijana anayedaiwa kujaribu kuiba pombe ya whisky. 

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 23, alidaiwa kujaribu kuiba pombe yenye thamani ya KSh1,800 kutoka kwa Duka Kuu la Naivas. Uamuzi wa Hakimu Mkuu Atambo ulifuatia mazungumzo mafupi yaliyojaa maswali, ushauri, na msukumo wa suluhu la vitendo badala ya adhabu. 

Kwa nini Hakimu wa Thika alikataa kumtia hatiani mwanafunzi? Alipouliza kuhusu thamani ya whisky, mwendesha mashtaka alijibu kuwa ni KSh1,000 kabla ya kusahihisha na kugundua kuwa KSh1,800 zilionekana kwenye karatasi ya mashtaka. 

Alimkumbusha kijana huyo kwamba kosa dogo mara nyingi hukua na kuwa mzigo wa muda mrefu mara moja linaporekodiwa kama hatia. 

Baada ya kuuliza na kuthibitisha umri wake, Atambo alimwambia bado ana maisha marefu na aepuke makosa ambayo yamesalia kwenye faili rasmi. "Wameandika KSh1,800. Unajua ikifika kwa charge sheet inakuwa more expensive. Si uwalipe tu, tuachane na story nyingi, ju hii itakuwa record of previous conviction. Uko na miaka mingapi? Miaka 23, bado wewe ni mchanga sana," alisema.

Mwanafunzi huyo aliiambia mahakama kuwa alipendelea kulipa pesa hizo badala ya kufungwa jela, lakini alikosa pesa kwa vile hakuwa na kazi. Alipouliza ikiwa kuna mtu yeyote alikuja kumsaidia kulipa dhamana ya pesa taslimu, alisema binamu yake alikuwa akielekea kortini.

Kisha akabadilisha mjadala, akieleza kwamba alitaka kumtia hatiani kwa kutumia chupa ya whisky ya John Barr. "Je, hutaki ulipe pesa za duka kuu sasa. Nikuwachilie. Wamesema KSh 1,800; whisky inaitwa nini? Unajua hii inaitwa John Barr Whisky. Sitaki ujibu maombi yako na kukuhukumu kwa sababu ya chupa ya whisky," Atambo aliambia mahakama. 

Jinsi gani Hakimu wa Thika alimwokoa mwanafunzi kutoka katika hatia Akiwageukia mawakili waliokuwepo kortini, Atambo alihoji wangeweza kumfanyia nini kwani alikuwa kijana anayehitaji mwelekeo. 

Mawakili hao walisema walikubaliana na hakimu, wakieleza kuwa kiasi hicho kilitakiwa kumalizwa na duka kubwa. 

Hakimu Atambo aliwakazia zaidi na kuwakumbusha madai yao ya mara kwa mara kuhusu kuwashauri vijana. "Wakili unamfahamu huyo? Humjui. 

Lakini huyu hapa mtoto wa kiume mwenzako. Unaweza kumfanyia nini?" aliuliza. Hakimu huyo alionekana kuhalalisha kitendo cha mwanafunzi huyo, na kuongeza kuwa kuna uwezekano alitaka muda mfupi wa kupumzika na akaishia kufanya uamuzi mbaya. 

Kundi la mawakili lilikubali kukusanya pesa ili kupata KSh1,800 huku wakisubiri binamu kuwasili. 

Wakili mmoja alisema maafisa wangemrejesha kwenye seli huku wakishauriana jinsi ya kulipa kiasi hicho. 

Hakimu Atambo alitumia muda huo kumtia moyo kujifunza kutokana na usaidizi ulioonyeshwa na wataalamu wakubwa katika chumba hicho. 

Alimweleza mwanafunzi kwamba hatia ingechafua rekodi zake na kupunguza fursa za siku zijazo. "Unaona sasa hawa ni kaka zako wakubwa. Wanajua maana yake unapoiba whisky tu ili upate wakati mzuri na kupumzika. Wakufanyie kitu maana nikikutia hatiani itachafua rekodi yako. Ona ni sawa," aliongeza. 

Alimwagiza awasiiane na binamu yake na akamhakikishia kwamba mawakili walikuwa tayari kumsaidia kulipa kiasi hicho. Mpangilio huo ulimaanisha kuwa mwanafunzi angefidia duka kuu bila kupokea rekodi ya uhalifu. 

MABASI YA ESTER SIO YANGU WALA MKE WANGU: MWIGULU

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba

 Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amevunja ukimya kuhusu uvumi unaoenezwa na baadhi ya watu kwamba mabasi ya kampuni ya Ester ni mali yake akisema jambo hilo sio la kweli na kuwataka Watanzania kutokubali kila wanachoelezwa.

“Siku hizi watu hawaogopi hata kusingizia jambo unakuta mtu hafanyi hata utafiti juu ya mtu anayetaka kumsema, juzi juzi nikasikia tumechoma magari ya Ester ya mbunge wa Iramba Magharibi, magari yake yanaitwa Ester ameyaita Ester jina la mke wake,”…

“Mke wangu mimi haitwi Ester anaitwa Neema, wanasema basi kama sio ya mke wake yatakuwa ya mama yake mama yangu binti wa kiislamu anaitwa Asha Ramadhani Mohamed,”


Dk.Mwigulu ambaye ametoa ufafanuzi huo IJUMAA ya Novemba 21, 2025 wakati akizungumza na mamia ya wananchi kwenye viwanja vya Bombadia Manispaa ya Singida, amesema yeye amezaliwa katika familia ya kifugaji ambayo huruhusiwi hata kufanya biashara ya miwa hivyo hajawahi kufanya biashara yeyote.

“Nimeingia huku serikalini uwekezaji mkubwa ninaoufanya ni kusomesha watoto na nina kundi la watoto zaidi ya 500 ninaowasomesha, nimewekeza kwenye huduma za watu,”amesema Dk.Mwigulu.

MBUNGE JIMBO LA KIBAHA VIJIJINI ATUA KWA KISHINDO NA KUTEMA CHECHE KWA WANANCHI

 


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA 


Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijiji Homoud Jumaa ameahidi  kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi (CCM)  kwa vitendo  ikiwemo kusimamia suala zima la kuwahudumia wananchi ipasavyo katika  mambo mbali mbali  kwa ajili ya kuwaletea chacu ya maendeleo katiika nyanja tofauti.

Jumaa ameyabainisha hayo wakati wa halfa fupi ya kumpokea rasmi kutokea Mkoani Dodoma ikiwa ni siku chache  zimepita baada ya kuapishwa rasmi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini  ambapo sherehe hiyo imehudhuliwa na na viongozi wa chama cha mapinduzi, wananchama pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti.

Mbunge huyo amesema kwamba kwa sasa uchaguzi umeshamalizika na kwamba kitu kikubwa amewaomba wanachama wote na wananchi kuhakikisha kwamba wadumisha hali ya amani na utulivu wa nchi na kuepukana na vurugu ambazo hazina maana na badala yake washikamane katika kukijenga chama pamoja na kushiriki kikamilifu katika mambo ya kimaendeleo.

"Nawashukuru kwa dhati viongozi wangu wa chama cha mapinduzi, wanachama wa ccm pamoja na wananchi wote kwa kuweza kuniamini kwa mara nyingine na kuweza kunipitisha tena kuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini kitu kikubwa ambacho ninaweza kuwaahidi ni kuendelea kutoa ushirikianio wa hali na mali katika kuhakikisha  ninawaletea maendeleo mbali mbali,"amesema Jumaa.  

Katika hatua nyiingine   Mbunge huyo amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. kwa kuweza kuchaguliwa kwa kishindo pamoja na kuweza kutoa hotuba yake nzuri ambayo imelenga kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi katika sekta mbali mbali.

Kwa upande wake Diwani mteule wa kata ya Kwala Mansuri Kisebengo amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini kwa kuweza kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi na kwamba ana imani kubwa wataweza kuwatumikia wananchi na kuwaletea chachu ya maendeleo.

Nao baadhi ya wananchi ambao wamepata fursa ya kuhudhulia katika halfa hiyo wamesema kwamba wana imani kubwa na serikali mpya  ya awamu  ya sita  pamoja na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo la Kibaha vijijini  Hamoud Jumaa kwani ataweza kuleta mafanikio ya kimaendeleo  kwa wananchi wake.

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijni Mhe. Hamoud Juma amepokelewa kwa kishindo kikubwa na viongozi CCM, wananchama pamoja na wananchi sambamba na madiwani  mbali mbali za Jimbo la KIbaha vijijini.

Monday, October 27, 2025

SERIKALI MKOA WA PWANI YAJIIMARISHA KWA ULINZI NA USALAMA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 VICTOR MASANGU, PWANI ... HABARI ..OCTOBA 27 /2025

SERIKALI Mkoa wa Pwani imesema kwamba imejiandaa  vya kutosha hususan katika hali ya ulinzi na usalama  katika kuelekea katika uchagzuo mkuu wa mwaka 2025 ambaop unatarajiwa kufanyika  octoba 29 mwaka huu ambayo itakuwa ni siku ya jumatano ya wiki hii.

Hayo yamebaishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge wakati akizunhgumza na waandishi wa habari  ofisini kwake kuhusiana na maandalizi ya kuelekea katika uchagzuzi huo ambapo amewaahimiza wanananchi wote wenye sifa  kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Saturday, October 25, 2025

WANANCHI MWANZA WAHIMIZA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 

Makundi mbalimbali ya wananchi jijini Mwanza yamejitokeza kwa wingi na kushiriki kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Kongamano hilo limeandaliwa na makundi hayo ambayo ni pamoja na machinga, bodaboda, wamiliki wa daladala, mama lishe na watu wenye ulemavu chini ya mlezi wao, Stanslaus Mabula ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana kwa awamu mbili kuanzia mwaka 2015/ 20225.

Katibu wa wamiliki wa daladala Mkoa wa Mwanza, Hussein Mosha akihimiza wananchi kulinda amani wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025.
Akizungumza kwenye kongamano hilo lililofanyika Jumamosi Oktoba 25, 2025 katika uwanja wa Nyamagana, Katibu wa wamiliki wa daladala Mkoa wa Mwanza, Hussein Mosha amesema Mwanza wamejiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani na utulivu.

"Niwaombe kila mmoja tuendelee kudumisha amani ya nchi yetu, bila amani hata pikipiki zetu hatuwezi kuziendesha, amani yetu ndiyo maisha yetu" amesema Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mkoa wa Mwanza, Mohamed Idd akihimiza wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani.

Naye Katibu wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Zuena Mahamudu amewahimiza wananchi kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi na badala yake wakashiriki zoezi la kupiga kura kwa wingi kwa mstakabali wa maisha yao.

Kwa upande wake mlezi wa makundi maalum ya wananchi walioandaa kongamano hilo, Stanslaus Mabula ambaye ni mbunge wa Nyamagana aliyemaliza muda wake amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura kwa amani ili kuwachagua viongozi bora watakaowavusha kimaendeleo.

Katibu wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Zuena Mahamudu akizungumza kwenye kongamano hilo na kuhimiza wananchi kujitokeza kwa amani kupiga kura.
Mwenyekiti wa madereva wa daladala Mkoa wa Mwanza, Mjarifu Manyasi akihimiza wananchi kujitokeza kwa amani kushiriki uchaguzi Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo akihimiza amani kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Mwanza, Mohamed Idd akihamasisha wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Mlezi wa makundi maalum Nyamagana, Stanslaus Mabula akihimiza wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Mlezi wa makundi maalum Nyamagana, Stanslaus Mabula akihimiza wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Mlezi wa makundi maalum Nyamagana, Stanslaus Mabula akihimiza wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Makundi mbalimbali ikiwemo bodaboda wakiwa kwenye kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.
Makundi mbalimbali ikiwemo bodaboda wakiwa kwenye kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.
Bodaboda wakitoka uwanja wa Nyamagana baada ya kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.


Kongamano la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 limeambatana na kaulimbiu isemayo, "Amani Yetu, Maisha Yetu".